Methali 16:13-27 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Mfalme hupendelea mtu asemaye kwa unyofu;humpenda mtu asemaye ukweli.

14. Hasira ya mfalme ni kama mjumbe wa kifo;mtu mwenye busara ataituliza.

15. Uso wa mfalme ukingaa kuna uhai;wema wake ni kama wingu la masika.

16. Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu;kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha.

17. Njia ya wanyofu huepukana na uovu;anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake.

18. Kiburi hutangulia maangamizi;majivuno hutangulia maanguko.

19. Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini,kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.

20. Anayezingatia mafundisho atafanikiwa;heri mtu yule anayemtumainia Mwenyezi-Mungu.

21. Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili;neno la kupendeza huwavutia watu.

22. Hekima ni chemchemi ya uhai kwake aliye nayo,bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu.

23. Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara;huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia.

24. Maneno mazuri ni kama asali;ni matamu rohoni na yenye kuupa mwili afya.

25. Mtu aweza kuona njia yake kuwa sawa,lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo.

26. Hamu ya chakula humhimiza mfanyakazi,maana njaa yake humsukuma aendelee.

27. Mtu mwovu hupanga uovu;maneno yake ni kama moto mkali.

Methali 16