Methali 14:17-30 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Mwenye kuwaka hasira haraka hutenda kipumbavu,lakini mwenye busara ana uvumilivu.

18. Wajinga hurithi upumbavu,lakini wenye busara hutuzwa taji ya maarifa.

19. Waovu watapiga magoti mbele ya watu wema,watu wabaya mlangoni mwa waadilifu.

20. Maskini huchukiwa hata na jirani yake,lakini tajiri ana marafiki wengi.

21. Anayemdharau jirani yake ni mwenye dhambi,bali ana heri aliye mwema kwa maskini.

22. Anayepanga maovu kweli anakosea!Wanaopanga kutenda mema hufadhiliwa.

23. Bidii katika kila kazi huleta faida,lakini maneno matupu huleta umaskini.

24. Mali ni taji ya fahari ya wenye hekima,lakini ujinga ni shada la wapumbavu.

25. Shahidi wa kweli huokoa maisha,lakini msema uongo ni msaliti.

26. Amchaye Mwenyezi-Mungu ana tumaini imara,na watoto wake watapata kimbilio salama.

27. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni chemchemi ya uhai;humwezesha mtu kuepa mitego ya kifo.

28. Fahari ya mfalme ni wingi wa watu wake,lakini bila watu mtawala huangamia.

29. Mtu asiye mwepesi wa hasira ana busara kubwa,lakini akasirikaye upesi hukuza upumbavu.

30. Amani rohoni humpa mtu afya,lakini tamaa huozesha mifupa.

Methali 14