Methali 14:12-27 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Njia unayodhani kuwa ni sawa,mwishoni yaweza kukuongoza kwenye kifo.

13. Huzuni yaweza kufichika katika kicheko;baada ya furaha huja majonzi.

14. Mtu mpotovu atavuna matunda ya mwenendo wake,naye mtu mwema atapata tuzo la matendo yake.

15. Mjinga huamini kila kitu anachoambiwa,lakini mwenye busara huwa na tahadhari.

16. Mwenye hekima ni mwangalifu na huepa uovu,lakini mpumbavu hajizuii wala hana uangalifu.

17. Mwenye kuwaka hasira haraka hutenda kipumbavu,lakini mwenye busara ana uvumilivu.

18. Wajinga hurithi upumbavu,lakini wenye busara hutuzwa taji ya maarifa.

19. Waovu watapiga magoti mbele ya watu wema,watu wabaya mlangoni mwa waadilifu.

20. Maskini huchukiwa hata na jirani yake,lakini tajiri ana marafiki wengi.

21. Anayemdharau jirani yake ni mwenye dhambi,bali ana heri aliye mwema kwa maskini.

22. Anayepanga maovu kweli anakosea!Wanaopanga kutenda mema hufadhiliwa.

23. Bidii katika kila kazi huleta faida,lakini maneno matupu huleta umaskini.

24. Mali ni taji ya fahari ya wenye hekima,lakini ujinga ni shada la wapumbavu.

25. Shahidi wa kweli huokoa maisha,lakini msema uongo ni msaliti.

26. Amchaye Mwenyezi-Mungu ana tumaini imara,na watoto wake watapata kimbilio salama.

27. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni chemchemi ya uhai;humwezesha mtu kuepa mitego ya kifo.

Methali 14