Mathayo 9:2-8 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako.”

3. Baadhi ya waalimu wa sheria wakaanza kufikiri, “Mtu huyu anamkufuru Mungu!”

4. Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, “Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu?

5. Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, utembee?’

6. Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo duniani wa kuwasamehe watu dhambi.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako.”

7. Huyo mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake.

8. Watu wote katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo.

Mathayo 9