2. Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.
3. Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta.
4. Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao.
5. Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wasichana wote walisinzia, wakalala.
6. Usiku wa manane kukawa na kelele: ‘Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.’
7. Hapo wale wasichana wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao.
8. Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: ‘Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.’
9. Lakini wale wenye busara wakawaambia, ‘Hayatatutosha sisi na nyinyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!’
10. Basi, wale wasichana wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wasichana waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la harusi, kisha mlango ukafungwa.
11. Baadaye wale wasichana wengine wakaja, wakaita: ‘Bwana, Bwana, tufungulie!’
12. Lakini yeye akawajibu, ‘Nawaambieni kweli, siwajui nyinyi.’”
13. Kisha Yesu akasema, “Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.
14. “Wakati huo itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ngambo: Aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake.
15. Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: Mmoja fedha talanta tano, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.
16. Mara yule aliyekabidhiwa fedha talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.
17. Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.