Mathayo 24:7-19 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi.

8. Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto.

9. “Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa sababu ya jina langu.

10. Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana.

11. Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi.

12. Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia.

13. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.

14. Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.

15. “Basi, mtakapoona ‘Chukizo Haribifu lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake),

16. hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani.

17. Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake.

18. Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.

19. Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!

Mathayo 24