12. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya.
13. Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’”
14. Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.”
15. Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake.
16. Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako.
17. Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?”
18. Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu?
19. Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha.
20. Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?”
21. Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.”
22. Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.
23. Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu.