11. Yesu akawaambia, “Si wote wanaoweza kulipokea fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu.
12. Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: Wengine ni kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na wengine wameamua kutooa kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee.”
13. Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea.
14. Yesu akasema, “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa.”
15. Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo.
16. Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, “Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uhai wa milele?”
17. Yesu akamwambia, “Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uhai, shika amri.”
18. Yule mtu akamwuliza, “Amri zipi?” Yesu akasema, “Usiue, Usizini, Usiibe, Usitoe ushahidi wa uongo,
19. Waheshimu baba yako na mama yako; na, Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”