Mathayo 15:3-17 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Yesu akawajibu, “Kwa nini nanyi hamjali sheria ya Mungu ila mnapendelea mapokeo yenu wenyewe?

4. Mungu amesema: ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na ‘Anayemtukana baba yake au mama yake, lazima auawe.’

5. Lakini nyinyi mwafundisha ati mtu akiwa na kitu ambacho angeweza kumsaidia nacho baba yake au mama yake, lakini akasema: ‘Kitu hiki nimemtolea Mungu,’

6. basi, hapaswi tena kumheshimu baba yake! Ndivyo mnavyodharau neno la Mungu kwa kufuata mafundisho yenu wenyewe.

7. Enyi wanafiki! Isaya alitabiri sawa kabisa juu yenu:

8. ‘Mungu asema: Watu hawa huniheshimu kwa maneno tu,lakini mioyoni mwao wako mbali nami.

9. Kuniabudu kwao hakufai,maana mambo wanayofundisha ni maagizo ya kibinadamu tu.’”

10. Yesu aliuita ule umati wa watu, akawaambia, “Sikilizeni, mkaelewe!

11. Kitu kinachomtia mtu unajisi si kile kiingiacho kinywani, bali kile kitokacho kinywani. Hicho ndicho kimtiacho mtu unajisi.”

12. Kisha wanafunzi wakamwendea, wakamwambia, “Je, unajua kwamba Mafarisayo walichukizwa waliposikia maneno yako?”

13. Lakini yeye akawajibu, “Kila mmea ambao Baba yangu aliye mbinguni hakupanda, utangolewa.

14. Waacheni wenyewe! Wao ni vipofu, viongozi wa vipofu; na kipofu akimwongoza kipofu, wote wawili hutumbukia shimoni.”

15. Petro akasema, “Tufafanulie huo mfano.”

16. Yesu akasema, “Hata nyinyi hamwelewi?

17. Je, hamwelewi kwamba kila kinachoingia kinywani huenda tumboni na baadaye hutolewa nje chooni?

Mathayo 15