Mathayo 12:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Wakati huo, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano siku ya Sabato. Basi, wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakala punje zake.

2. Mafarisayo walipoona hayo, wakamwambia Yesu, “Tazama, wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanya siku ya Sabato.”

3. Yesu akawajibu, “Je, hamjasoma alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa?

4. Yeye aliingia katika nyumba ya Mungu akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Yeye wala hao wenzake hawakuruhusiwa kula mikate hiyo isipokuwa tu makuhani peke yao.

5. Au je, hamjasoma katika kitabu cha sheria kwamba kila siku ya Sabato makuhani huivunja sheria hekaluni, lakini hawafikiriwi kuwa na hatia?

6. Basi, nawaambieni kwamba hapa pana kikuu kuliko hekalu.

7. Kama tu mngejua maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma wala si tambiko,’ hamngewahukumu watu wasio na hatia.

8. Maana Mwana wa Mtu ana uwezo juu ya Sabato.”

9. Yesu alitoka hapo, akaenda katika sunagogi lao.

Mathayo 12