16. “Sasa, mimi nawatuma nyinyi kama kondoo kati ya mbwamwitu. Muwe na busara kama nyoka, na wapole kama njiwa.
17. Jihadharini na watu, maana watawapeleka nyinyi mahakamani na kuwapiga viboko katika masunagogi yao.
18. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu, mpate kunishuhudia kwao na kwa watu wa mataifa.
19. Basi, watakapowapeleka nyinyi mahakamani, msiwe na wasiwasi mtasema nini au namna gani; wakati utakapofika, mtapewa la kusema.
20. Maana si nyinyi mtakaosema, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.
21. “Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe, na baba atamsaliti mwanawe, nao watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.
22. Watu wote watawachukieni nyinyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ndiye atakayeokolewa.
23. “Watu wakiwadhulumu katika mji mmoja, kimbilieni mji mwingine. Kweli nawaambieni, hamtamaliza ziara yenu katika miji yote ya Israeli kabla Mwana wa Mtu hajafika.