1. Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa uwezo wa kuwafukuza pepo wachafu na kuponya magonjwa na maradhi yote.
2. Majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya: Wa kwanza ni Simoni aitwaye Petro, na Andrea ndugu yake; Yakobo mwana wa Zebedayo, na Yohane ndugu yake;
3. Filipo na Bartholomayo, Thoma na Mathayo aliyekuwa mtozaushuru; Yakobo mwana wa Alfayo, na Thadayo;
4. Simoni Mkanaani, na Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.
5. Yesu aliwatuma hao kumi na wawili na kuwapa maagizo haya: “Msiende kwa watu wa mataifa mengine, wala msiingie katika miji ya Wasamaria.