23. Kwa maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi ninamwabudu alinitokea,
24. akaniambia: ‘Paulo, usiogope! Ni lazima utasimama mbele ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri nawe wasiangamie.’
25. Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa.
26. Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa fulani.”
27. Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku na huko katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi kuwa karibu na nchi kavu.
28. Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arubaini. Baadaye wakapima tena wakapata mita thelathini.
29. Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba, waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi.
30. Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa mbele wa meli.
31. Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari wake, “Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka.”
32. Hapo wale askari walizikata kamba zilizokuwa zimeshikilia ule mtumbwi, wakauacha uchukuliwe na maji.
33. Karibu na alfajiri, Paulo aliwahimiza wote wale chakula: “Kwa siku kumi na nne sasa mmekuwa katika mashaka na bila kula; hamjala kitu chochote.