17. Tulipofika Yerusalemu, ndugu waumini walitupokea vizuri sana.
18. Kesho yake Paulo alikwenda pamoja nasi kumwamkia Yakobo, na wazee wote wa kanisa walikuwapo pia.
19. Baada ya kuwasalimu, Paulo aliwapa taarifa kamili kuhusu yote Mungu aliyokuwa ametenda kati ya watu wa mataifa kwa njia ya utumishi wake.
20. Waliposikia hayo, walimtukuza Mungu. Kisha wakamwambia Paulo, “Ndugu, unaweza kuona kwamba kuna maelfu ya Wayahudi ambao sasa wamekuwa waumini na wote hao wanazingatia sheria.
21. Wamepata habari zako kwamba umekuwa ukiwafundisha Wayahudi wanaoishi miongoni mwa watu wa mataifa mengine kuwa wasiijali sheria, wasiwatahiri watoto wao na kwamba wasizifuate mila za Wayahudi.