4. Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: ‘Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu,
5. lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!’”
6. Basi, Bwana akaendelea kusema, “Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya.
7. Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza?
8. Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?”
9. Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine.
10. “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali: Mmoja Mfarisayo, na mwingine mtozaushuru.
11. Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: ‘Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: Walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtozaushuru.
12. Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.’
13. Lakini yule mtozaushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: ‘Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.’
14. Nawaambieni, huyu mtozaushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa.”
15. Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.