14. Nawaambieni, huyu mtozaushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa.”
15. Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.
16. Lakini Yesu akawaita kwake akisema: “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.
17. Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika ufalme huo.”
18. Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, “Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uhai wa milele?”
19. Yesu akamwambia, “Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
20. Unazijua amri: ‘Usizini; Usiue; Usiibe; Usitoe ushahidi wa uongo; Waheshimu baba yako na mama yako.’”