4. Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu, wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu?
5. Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao.”
6. Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini shambani mwake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja.
7. Basi, akamwambia mfanyakazi wake: ‘Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, bila kupata chochote. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?’
8. Lakini yeye akamjibu: ‘Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea.
9. Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata.’”
10. Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato.
11. Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima.
12. Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, “Mama, umeponywa ugonjwa wako.”
13. Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu.