5. Tena Farao akasema, “Hawa watu wenu ni wengi kuliko wananchi; mnataka waache kufanya kazi!”
6. Siku hiyohiyo Farao aliwaamuru wanyapara pamoja na wasimamizi, akasema,
7. “Tangu leo msiwape watu hawa nyasi za kutengenezea matofali kama ilivyo kawaida. Wao wenyewe watakwenda kujitafutia.
8. Lakini idadi ya matofali yanayotengenezwa kila siku iwe ileile, wala lisipungue hata tofali moja, kwa kuwa watu hawa ni wavivu ndio maana wanapiga kelele: ‘Tuache twende tukamtambikie Mungu wetu.’
9. Wazidishieni watu hawa kazi ngumu ili waitolee jasho na kuacha kusema maneno ya uongo.”
10. Basi, wanyapara na wasimamizi wa watu wakatoka na kuwaambia watu, “Farao anasema hivi, ‘Sitawapeni nyasi.
11. Nendeni nyinyi wenyewe mkatafute popote mtakapoweza kuzipata, na wala kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’”
12. Basi, watu wote wakatawanyika kila mahali nchini Misri wakitafuta nyasi za kutengenezea matofali.
13. Nao Wanyapara wakakazana wakisema, “Timizeni kazi yenu ya kila siku kama hapo awali mlipoletewa nyasi.”
14. Wanyapara Wamisri wakawapiga wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa kusimamia kazi wakisema, “Kwa nini hamtimizi kazi yenu na kufikisha idadi ileile ya matofali kama awali?”
15. Ndipo wasimamizi wa Waisraeli walipomwendea Farao, wakamlilia wakisema, “Kwa nini unatutenda hivi sisi watumishi wako?