30. Kisha walitengeneza pambo la dhahabu safi kwa ajili ya taji takatifu na kuchora juu yake kama wachoravyo mhuri, “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.”
31. Kisha wakalifunga mbele ya kile kilemba kwa ukanda wa rangi ya buluu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
32. Basi, kazi yote ya hema la mkutano ikamalizika. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
33. Wakamletea Mose hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote, vikonyo vyake, mbao zake, pau zake, nguzo zake na vikalio vyake;
34. kifuniko cha ngozi za kondoo dume na mbuzi kilichotiwa rangi nyekundu, pazia la mahali patakatifu,
35. sanduku la agano, mipiko yake na kiti cha rehema;
36. meza na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mungu;
37. kinara cha taa cha dhahabu safi, taa zake, vyombo vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa hizo;
38. madhabahu ya dhahabu; mafuta ya kupaka, ubani wenye harufu nzuri, na pazia la mlango wa hema;