26. “Utatengeneza pau za mjohoro; pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema,
27. na pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi.
28. Upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema utapenya katikati toka mwisho huu hadi mwisho mwingine wa hema.
29. Mbao zote utazipaka dhahabu na kuzifanyia pete za dhahabu zitakazoshikilia hizo pau, ambazo pia utazipaka dhahabu.
30. Hivyo utalitengeneza hema hilo kulingana na mfano niliokuonesha mlimani.
31. “Utatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo utalitarizi kwa ustadi kwa viumbe wenye mabawa.
32. Utalitundika pazia kwenye nguzo nne za mjohoro zilizopakwa dhahabu, zenye kulabu za dhahabu na vikalio vinne vya fedha.
33. Utalitundika pazia hilo kwenye vifungo, kisha ulilete lile sanduku la ushuhuda humo ndani kukiwa na vibao viwili vya mawe, nyuma ya pazia hilo. Pazia hilo litatenga mahali patakatifu na mahali patakatifu sana.
34. Ndani ya mahali patakatifu utakiweka kile kiti cha rehema juu ya sanduku la maamuzi.
35. Ile meza ya mjohoro utaiweka upande wa nje wa pazia hilo, na kile kinara cha taa utakiweka upande wa kusini wa hema, mkabala wa meza. Meza hiyo itakuwa upande wa kaskazini.
36. “Kwa ajili ya mlango wa hema utatengeneza pazia zito kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri.
37. Vilevile utatengeneza nguzo tano za mjohoro na kuzipaka dhahabu. Nguzo hizo zitakuwa na kulabu za dhahabu, na kila moja itakuwa na tako la shaba.