Kutoka 22:6-15 Biblia Habari Njema (BHN)

6. “Mtu akiwasha moto nao ukachoma miti ya miiba na kusambaa hadi kuteketeza miganda ya nafaka, au nafaka ya mtu mwingine ambayo bado haijavunwa, au shamba lote likateketea, aliyewasha moto huo lazima alipe hasara hiyo yote.

7. “Mtu akimwachia mwenzake fedha au mali nyingine amtunzie, kisha ikaibiwa nyumbani mwake, mwizi akipatikana lazima alipe thamani yake mara mbili.

8. Lakini mwizi asipopatikana, mwenye nyumba atakaribia mbele za Mungu ili kuthibitisha kwamba hakuhusika na wizi wa mali ya mwenzake.

9. “Pakiwa na ubishi juu ya ng'ombe, au punda, au kondoo, au mavazi, au kitu chochote kilichopotea ambacho kila mmoja anadai ni chake, wanaohusika wataletwa mbele za Mungu. Yule ambaye Mungu ataamua amekosa, atamlipa mwenzake mara mbili.

10. “Mtu akimkabidhi mwenzake punda, ng'ombe, kondoo au mnyama mwingine yeyote amtunzie, na mnyama huyo akafa au akaumia au akachukuliwa bila mtu yeyote kushuhudia,

11. kiapo mbele ya Mwenyezi-Mungu kitaamua kati yao, kuonesha kwamba huyo aliyekabidhiwa hakuhusika na wizi wa mali ya mwenzake. Mwenye mnyama huyo atakubali hicho kiapo, na huyo mwenzake hatalipa malipo yoyote.

12. Lakini kama aliibiwa kwake, ni lazima amlipe mwenyewe.

13. Kama huyo mnyama aliraruliwa na wanyama wa porini, huyo mtu aliyekuwa amekabidhiwa lazima amlete kama ushahidi. Hatalipa malipo yoyote kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama wa porini.

14. “Mtu akiazima mnyama kwa mwenzake, kisha mnyama huyo akaumia au akafa wakati mwenyewe hayuko, aliyeazima mnyama huyo ni lazima alipe kikamilifu.

15. Lakini kama mwenyewe alikuwako, basi aliyemwazima hatalipa chochote. Kama alikuwa ni mnyama aliyekodishwa, mwenyewe ataikubali tu bei ya kukodisha.

Kutoka 22