11. kiapo mbele ya Mwenyezi-Mungu kitaamua kati yao, kuonesha kwamba huyo aliyekabidhiwa hakuhusika na wizi wa mali ya mwenzake. Mwenye mnyama huyo atakubali hicho kiapo, na huyo mwenzake hatalipa malipo yoyote.
12. Lakini kama aliibiwa kwake, ni lazima amlipe mwenyewe.
13. Kama huyo mnyama aliraruliwa na wanyama wa porini, huyo mtu aliyekuwa amekabidhiwa lazima amlete kama ushahidi. Hatalipa malipo yoyote kwa ajili ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama wa porini.
14. “Mtu akiazima mnyama kwa mwenzake, kisha mnyama huyo akaumia au akafa wakati mwenyewe hayuko, aliyeazima mnyama huyo ni lazima alipe kikamilifu.
15. Lakini kama mwenyewe alikuwako, basi aliyemwazima hatalipa chochote. Kama alikuwa ni mnyama aliyekodishwa, mwenyewe ataikubali tu bei ya kukodisha.
16. “Mtu akimshawishi bikira ambaye hajaposwa, akalala naye, lazima atoe mahari na kumwoa msichana huyo.
17. Baba wa huyo msichana akikataa katakata kumwoza binti yake, mtu huyo atalipa fedha ya mahari inayostahili msichana aliye bikira.
18. “Usimwache mwanamke mchawi aishi.
19. “Anayezini na mnyama lazima auawe.
20. “Anayemtolea tambiko mungu mwingine badala ya Mwenyezi-Mungu pekee, lazima aangamizwe kabisa.
21. “Msimdhulumu mgeni wala kumtesa, maana nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri.
22. Msimtese mjane au yatima.
23. Kama mkiwadhulumu hao nao wakanililia, hakika nitakisikiliza kilio chao,
24. na hasira yangu itawaka, nami nitawaueni kwa upanga, na wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu yatima.
25. “Ukimkopesha fedha mtu yeyote miongoni mwa watu wangu walio maskini, usiwe kwake kama mdai, wala usimtoze riba.
26. Ukilichukua vazi la mwenzako kuliweka rehani, lazima umrudishie kabla ya jua kutua,
27. kwa kuwa hiyo ndiyo nguo yake ya pekee; ndiyo atakayojifunika nayo. Au wadhani atalalia nini? Akinililia nitamsikiliza, maana mimi ni mwenye huruma.
28. “Usimtukane Mungu, wala kumlaani mkuu wa watu wako.
29. “Usikawie kunitolea sehemu yangu kutokana na wingi wa mazao yako na divai yako. Mtanipa wazaliwa wenu wa kwanza wa kiume.