Kutoka 12:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, walipokuwa bado nchini Misri,

2. “Mwezi huu utakuwa kwenu mwezi wa kwanza wa mwaka.

3. Iambieni jumuiya yote ya Waisraeli kwamba mnamo siku ya kumi ya mwezi huu, mtachukua mwanakondoo mmoja kwa kila jamaa moja.

4. Kama jamaa moja ni ndogo mno hata isiweze kumaliza kondoo mmoja, itashirikiana na jamaa jirani kadiri ya idadi ya watu wake; kisha watachagua mnyama ambaye kila mtu ataweza kula.

5. Mwanakondoo huyo asiwe na kilema chochote, awe wa kiume na wa mwaka mmoja. Anaweza kuwa mwanakondoo au mwanambuzi.

6. Mtamweka mnyama huyo mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi huu. Siku hiyo, jumuiya yote ya Waisraeli watawachinja wanyama hao wakati wa jioni.

7. Kisha, watachukua damu ya hao wanyama na kupaka kwenye miimo na vizingiti vya kila nyumba watakamolia wanyama hao.

8. Wataila nyama hiyo usiku huohuo baada ya kuichoma; wataila pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga chungu za majani.

9. Imekatazwa kuila ikiwa mbichi au imechemshwa kwa maji, bali lazima ichomwe yote, pamoja na kichwa, miguu na nyama zake za ndani.

10. Hali kadhalika msibakize nyama yoyote mpaka asubuhi. Nyama yoyote itakayobaki hadi asubuhi mtaiteketeza motoni.

11. Na hivi ndivyo mtakavyomla mnyama huyo: Mtakuwa mmejifunga mikanda viunoni mwenu, mmevaa viatu na fimbo zenu mikononi. Tena mtamla kwa haraka. Hiyo ni Pasaka ya Mwenyezi-Mungu.

12. “Usiku huo, nitapita katika nchi ya Misri na kuwaua wazaliwa wa kwanza wa Misri, watu kwa wanyama. Nitaiadhibu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

13. Basi, ile damu itakuwa ishara yenu ya kuonesha nyumba mtakamokuwa. Nami nitakapoiona hiyo damu, nitawapita nyinyi, na hamtapatwa na dhara lolote wakati nitakapoipiga nchi ya Misri.

14. Vizazi hata vizazi mtaadhimisha tukio hilo kwa sikukuu kubwa kwa heshima yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Hilo litakuwa agizo la milele kwenu.”

Kutoka 12