4. Ndipo mkuu wa matowashi wa Ashuru alipowaambia, “Mwambieni Hezekia kuwa mfalme mkuu wa Ashuru anamwuliza, ‘Je, unategemea nini kwa ukaidi wako huo?
5. Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi?
6. Angalia! Sasa unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeuegemea. Hivyo ndivyo Farao, mfalme wa Misri alivyo, kwa wote wale wanaomtegemea.’
7. Lakini hata kama mkiniambia, ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,’ je, si huyohuyo ambaye Hezekia aliziharibu madhabahu zake na kuwaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, ‘Mnapaswa kuabudu mbele ya madhabahu hii?’
8. Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru; mimi nitawapatieni farasi 2,000, kama mtaweza kupata wapandafarasi.
9. Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu aliye na cheo cha chini sana wakati mnategemea Misri kupata magari ya vita na wapandafarasi!
10. Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia ‘Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!’”
11. Kisha Eliakimu, Shebna na Yoa wakamjibu mkuu wa matowashi, “Tafadhali sema nasi kwa lugha ya Kiaramu maana tunaielewa. Usiseme nasi kwa lugha ya Kiebrania kwa kuwa watu walioko ukutani wanasikia.”
12. Yule mkuu wa matowashi akawaambia, “Je unadhani bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu wenyewe tu? Maneno yangu ni pia kwa watu wanaokaa ukutani! Muda si muda wao kama vile nyinyi itawabidi kula mavi yao wenyewe na kunywa mikojo yao wenyewe!”
13. Kisha huyo mkuu wa matowashi akasimama, akapaza sauti na kusema kwa Kiebrania, “Sikilizeni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru!
14. Hiki ndicho anachosema mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye, kwa sababu hataweza kuwaokoa.
15. Msikubali awashawishi ili mumtegemee Mwenyezi-Mungu akisema, ‘Mwenyezi-Mungu hakika atatuokoa na mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’