Isaya 36:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mnamo mwaka wa kumi na nne wa utawala wa mfalme Hezekia, mfalme Senakeribu wa Ashuru aliishambulia miji yote yenye ngome ya Yuda na kuiteka.

2. Kisha mfalme wa Ashuru alimtuma jemadari mkuu kutoka Lakishi na jeshi kubwa kumwendea mfalme Hezekia. Jemadari alisimama karibu na mfereji wa bwawa lililoko upande wa juu katika barabara kuu inayoelekea uwanda wa Dobi.

3. Nao walilakiwa na Eliakimu mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa ikulu, Shebna aliyekuwa katibu, pamoja na mwandishi Yoa mwana wa Asafu.

4. Ndipo mkuu wa matowashi wa Ashuru alipowaambia, “Mwambieni Hezekia kuwa mfalme mkuu wa Ashuru anamwuliza, ‘Je, unategemea nini kwa ukaidi wako huo?

5. Je, unadhani kuwa maneno matupu ndiyo maarifa na nguvu katika vita? Ni nani unayemtegemea hata ukaniasi?

6. Angalia! Sasa unategemea Misri, utete uliovunjika ambao utamchoma mkono yeyote atakayeuegemea. Hivyo ndivyo Farao, mfalme wa Misri alivyo, kwa wote wale wanaomtegemea.’

7. Lakini hata kama mkiniambia, ‘Tunamtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,’ je, si huyohuyo ambaye Hezekia aliziharibu madhabahu zake na kuwaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, ‘Mnapaswa kuabudu mbele ya madhabahu hii?’

8. Basi, fanyeni mkataba na bwana wangu mfalme wa Ashuru; mimi nitawapatieni farasi 2,000, kama mtaweza kupata wapandafarasi.

9. Mwawezaje kumrudisha nyuma ofisa mmoja kati ya watumishi wa bwana wangu aliye na cheo cha chini sana wakati mnategemea Misri kupata magari ya vita na wapandafarasi!

10. Zaidi ya hayo, je, mnafikiri nimekuja bila amri ya Mwenyezi-Mungu ili kuishambulia na kuiangamiza nchi hii? Mwenyezi-Mungu ndiye aliyeniambia ‘Ishambulie nchi hii na kuiangamiza!’”

Isaya 36