Isaya 19:21-25 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Mwenyezi-Mungu atajijulisha kwa Wamisri na hapo ndipo Wamisri watakapomkiri na kumwabudu kwa kumtolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Hali kadhalika, watamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri ambazo watazitimiza.

22. Mwenyezi-Mungu atawaadhibu Wamisri na kuwaponya. Nao watamrudia, naye atayasikiliza maombi yao na kuwaponya.

23. Wakati huo, kutakuwa na barabara kuu kutoka nchi ya Misri hadi nchi ya Ashuru. Waashuru watawatembelea Wamisri, na Wamisri watawatembelea Waashuru; nao wote watamwabudu Mungu pamoja.

24. Wakati huo, Israeli itahesabiwa pamoja na Misri na Ashuru; mataifa haya matatu yatakuwa baraka kwa dunia yote.

25. Mwenyezi-Mungu wa majeshi atawabariki na kusema, “Wabarikiwe Wamisri watu wangu, kadhalika na Waashuru ambao ni ishara ya kazi yangu na Waisraeli walio mali yangu.”

Isaya 19