Isaya 19:14-24 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Mwenyezi-Mungu amewamwagia hali ya vurugu,wakawapotosha Wamisri katika mipango yao yote,wakawa kama mlevi anayeyumbayumba akitapika.

15. Hakuna mtu yeyote nchini Misri,kiongozi au raia, mashuhuri au duni,awezaye kufanya lolote la maana.

16. Siku ile watu wa Misri wataogopa kama wanawake. Watatetemeka kwa hofu watakapomwona Mwenyezi-Mungu wa majeshi ameunyosha mkono wake dhidi yao.

17. Yuda atakuwa tishio kubwa kwa Wamisri. Wote watakaoambiwa habari za Yuda wataingiwa na woga kwa sababu ya jambo aliloamua Mwenyezi-Mungu wa majeshi kuwatenda.

18. Siku hiyo lugha ya Kiebrania itatumika katika miji mitano ya Misri, na watu wa miji hiyo wataapa kuwa waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Mji mmojawapo utaitwa “Mji wa Jua.”

19. Siku hiyo, kutakuwa na madhabahu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu katikati ya nchi ya Misri, na nguzo iliyowekwa wakfu kwa Mungu kwenye mpaka wa Misri.

20. Madhabahu hiyo itakuwa ishara na ushuhuda kwake Mwenyezi-Mungu wa majeshi katika nchi ya Misri. Watu wakimlilia Mwenyezi-Mungu humo kwa sababu ya kukandamizwa, yeye atawapelekea mkombozi atakayewatetea na kuwakomboa.

21. Mwenyezi-Mungu atajijulisha kwa Wamisri na hapo ndipo Wamisri watakapomkiri na kumwabudu kwa kumtolea tambiko na sadaka za kuteketezwa. Hali kadhalika, watamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri ambazo watazitimiza.

22. Mwenyezi-Mungu atawaadhibu Wamisri na kuwaponya. Nao watamrudia, naye atayasikiliza maombi yao na kuwaponya.

23. Wakati huo, kutakuwa na barabara kuu kutoka nchi ya Misri hadi nchi ya Ashuru. Waashuru watawatembelea Wamisri, na Wamisri watawatembelea Waashuru; nao wote watamwabudu Mungu pamoja.

24. Wakati huo, Israeli itahesabiwa pamoja na Misri na Ashuru; mataifa haya matatu yatakuwa baraka kwa dunia yote.

Isaya 19