36. Wao walipewa kazi ya kutunza mbao za hema takatifu, mataruma, nguzo, vitako na vifaa vyote vya kushikilia hema; huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa juu yao.
37. Pia walihitajika kutunza nguzo za ua zilizouzunguka na vitako vyake, vigingi na kamba zake.
38. Mose na Aroni na wana wao walitakiwa kupiga kambi yao mbele ya hema takatifu upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua. Wajibu wao ulikuwa kutoa huduma kwenye mahali patakatifu kwa lolote lililohitajika kufanyika kwa ajili ya Waisraeli. Mtu mwingine yeyote aliyesogea karibu ilibidi auawe.
39. Idadi ya Walawi kulingana na familia zao, wanaume wote kuanzia watoto wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ambao Mose na Aroni waliwahesabu kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, ilikuwa watu 22,000.
40. Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Wahesabu kwa majina wazaliwa wa kwanza wa kiume wote wa Waisraeli kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi.
41. Nawe utatenga Walawi kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu; pia utatenga kwa ajili yangu mifugo yote ya Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa mifugo ya watu wa Israeli.”
42. Basi, Mose akawahesabu wazaliwa wa kwanza wote wa watu wa Israeli kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru.
43. Wazaliwa wote wa kwanza wa kiume kadiri ya hesabu ya majina, kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi, kufuata walivyohesabiwa, walikuwa 22,273.
44. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
45. “Sasa, watenge Walawi wote kuwa wangu badala ya wazaliwa wa kwanza wa Waisraeli. Kadhalika, watenge ng'ombe wa Walawi wote badala ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe wa Waisraeli. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
46. Kwa ajili ya fidia ya wazaliwa wa kwanza wa kiume wa watu wa Israeli 273, wanaozidi idadi ya wanaume Walawi,
47. utapokea kwa kila mwanamume fedha shekeli tano, kulingana na kipimo cha mahali patakatifu, ambayo ni sawa na gera ishirini,
48. na fedha hizo kwa ajili ya fidia ya hao waliozidi idadi yao utampa Aroni na wanawe.”