30. naye Elisafani, akiwa mkuu wa ukoo huo wa familia za Wakohathi.
31. Wajibu wao ulikuwa kulitunza sanduku la agano, meza, kinara cha taa, madhabahu, vyombo wanavyotumia makuhani mahali patakatifu na pazia; huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa zao.
32. Naye Eleazari mwana wa kuhani Aroni aliwekwa kuwa mkuu wa wakuu wa Walawi, na msimamizi wa wahudumu wote wa mahali patakatifu.
33. Familia za Wamahli na Wamushi zilitokana na Merari.
34. Hizi ndizo familia za Merari. Idadi yao kadiri ya hesabu ya wanaume wote kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ilikuwa watu 6,200.
35. Mkuu wa ukoo wa familia za Merari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hawa walitakiwa kupiga kambi yao upande wa kaskazini wa hema takatifu.
36. Wao walipewa kazi ya kutunza mbao za hema takatifu, mataruma, nguzo, vitako na vifaa vyote vya kushikilia hema; huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa juu yao.
37. Pia walihitajika kutunza nguzo za ua zilizouzunguka na vitako vyake, vigingi na kamba zake.
38. Mose na Aroni na wana wao walitakiwa kupiga kambi yao mbele ya hema takatifu upande wa mashariki kuelekea mawio ya jua. Wajibu wao ulikuwa kutoa huduma kwenye mahali patakatifu kwa lolote lililohitajika kufanyika kwa ajili ya Waisraeli. Mtu mwingine yeyote aliyesogea karibu ilibidi auawe.