15. “Wahesabu wana wa Lawi wote kulingana na koo zao na familia zao, kila mwanamume kuanzia watoto wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi.”
16. Basi, Mose akawahesabu kufuatana na neno la Mwenyezi-Mungu, kama alivyomwamuru.
17. Wafuatao ndio waliokuwa wana wa Lawi: Gershoni, Kohathi na Merari.
18. Na haya ndiyo majina ya wana wa Gershoni kwa kufuata familia zao: Libni na Shimei.
19. Wana wa Kohathi kwa kufuata familia zao: Amramu, Ishari, Hebroni na Uzieli.
20. Wana wa Merari kwa kufuata familia zao: Mahli na Mushi. Hizi zilikuwa jamaa za Walawi kulingana na koo zao.
21. Familia za Walibni na Washimei zilitokana na Gershoni; hizi ndizo zilizokuwa jamaa za Wagershoni.
22. Idadi yao kwa kadiri ya hesabu ya wanaume wote kuanzia waliokuwa na mwezi mmoja na zaidi ni 7,500.
23. Familia za Wagershoni, iliwapasa kupiga kambi yao upande wa magharibi, nyuma ya hema takatifu
24. naye Eliasafu mwana wa Laeli akiwa mkuu wa ukoo wa Wagershoni.
25. Kazi ya wana wa Gershoni ilikuwa kulitunza hema takatifu, hema pamoja na kifuniko chake, pazia la mlango wa hema la mkutano,
26. mapazia ya ua ulioko kati ya hema takatifu na madhabahu, na pazia la mlango wa ua, na kamba zake. Huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa zao.
27. Familia za Waamrami, Waishari, Wahebroni na Wauzieli zilitokana na Kohathi; hizi ndizo zilizokuwa jamaa za Wakohathi.
28. Kadiri ya hesabu ya wanaume wote kuanzia wenye umri wa mwezi mmoja na zaidi ilikuwa 8,600, waliohusika na huduma za mahali patakatifu.
29. Familia za wana wa Kohathi zilitakiwa kupiga kambi yao upande wa kusini wa mahali patakatifu,
30. naye Elisafani, akiwa mkuu wa ukoo huo wa familia za Wakohathi.
31. Wajibu wao ulikuwa kulitunza sanduku la agano, meza, kinara cha taa, madhabahu, vyombo wanavyotumia makuhani mahali patakatifu na pazia; huduma zote zilizohusu vitu hivi zilikuwa zao.
32. Naye Eleazari mwana wa kuhani Aroni aliwekwa kuwa mkuu wa wakuu wa Walawi, na msimamizi wa wahudumu wote wa mahali patakatifu.