Hesabu 29:5-24 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Tena mtatoa beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi ili kuwafanyia upatanisho.

6. Mtatoa vitu hivi licha ya ile sadaka ya kuteketezwa ya mwezi mpya na sadaka yake ya nafaka, na sadaka ya kila siku ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka zake za kinywaji kama inavyotakiwa kuwa harufu nzuri ipendezayo, ni sadaka kwa Mwenyezi-Mungu iliyoteketezwa kwa moto.

7. “Siku ya kumi ya mwezi wa saba mtafanya mkutano mtakatifu. Siku hiyo ni lazima mfunge na msifanye kazi.

8. Mtamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa kwa moto, harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali mmoja mchanga, kondoo dume mmoja, wanakondoo saba wa mwaka mmoja. Wote wasiwe na dosari.

9. Licha ya vitu hivi mtatoa sadaka ya unga safi uliochanganywa na mafuta kilo tatu pamoja na huyo fahali, kilo mbili pamoja na yule kondoo dume,

10. na kilo moja kwa kila mwanakondoo.

11. Mtatoa pia beberu mmoja kwa sadaka ya kuondoa dhambi licha ya sadaka ya kufanyiwa upatanisho, pamoja na sadaka ya kawaida ya kuteketezwa na sadaka yake ya nafaka na sadaka zake za kinywaji.

12. “Siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, mtafanya mkutano mtakatifu. Hamtafanya kazi siku hiyo. Mtaadhimisha sikukuu kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu kwa siku saba.

13. Mtatoa sadaka ya kuteketezwa kwa moto, iliyo harufu nzuri inayompendeza Mwenyezi-Mungu: Fahali wachanga kumi na watatu, kondoo madume wawili, wanakondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja. Wote wawe bila dosari.

14. Sadaka itakayoandamana nazo itakuwa unga safi uliochanganywa na mafuta: Kilo tatu kwa kila fahali, kilo mbili kwa kila kondoo,

15. na kilo moja kwa kila mwanakondoo.

16. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa, pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji.

17. “Siku ya pili mtatoa: Fahali wachanga kumi na wawili, kondoo madume wawili, wanakondoo wa kiume kumi na wanne, wa mwaka mmoja wasio na dosari.

18. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za vinywaji pamoja na wale fahali, kondoo na wanakondoo, kulingana na idadi yao.

19. Mtatoa pia beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya sadaka ya kuteketezwa ya kawaida pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji.

20. “Siku ya tatu mtatoa: Fahali kumi na mmoja, kondoo wawili, wanakondoo kumi na wanne wa mwaka mmoja, wasio na dosari.

21. Mtawatolea pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji kama ilivyotakiwa kulingana na idadi yao.

22. Vilevile mtatoa beberu mmoja kwa sadaka ya kuondoa dhambi, licha ya ile sadaka ya kawaida ya kuteketezwa pamoja na sadaka yake ya nafaka na sadaka yake ya kinywaji.

23. “Siku ya nne mtatoa: Fahali kumi, kondoo madume wawili, wanakondoo kumi na wanne, wasio na dosari.

24. Mtatoa pia sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji pamoja na hao fahali na kondoo na wanakondoo kulingana na idadi yao, kama inavyotakiwa.

Hesabu 29