20. Basi, Mungu akamjia Balaamu usiku huo, akamwambia, “Kama watu hawa wamekuja kukuita, nenda pamoja nao, lakini fanya tu kile nitakachokuambia.”
21. Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na hao maofisa.
22. Hasira ya Mungu iliwaka kwa sababu Balaamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akakabiliana naye njiani. Wakati huo Balaamu alikuwa amepanda punda wake akiwa na watumishi wake.
23. Basi, punda alimwona malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu amesimama njiani, ameshika upanga uliochomolewa alani mwake. Kwa hiyo aliiacha njia, akaenda pembeni. Balaamu akampiga huyo punda, akamrudisha njiani.
24. Kisha malaika huyo wa Mwenyezi-Mungu akatangulia mbele, akasimama mahali penye njia nyembamba, kati ya mashamba ya mizabibu na kuta pande zote mbili.