12. Mungu akamwambia Balaamu, “Usiende pamoja na watu hawa, wala usiwalaani watu hao maana wamebarikiwa.”
13. Basi, asubuhi yake Balaamu aliamka, akawaambia maofisa wa Balaki, “Rudini nchini mwenu, kwa maana Mwenyezi-Mungu hapendi kuniruhusu kwenda pamoja nanyi.”
14. Kwa hiyo maofisa wa Moabu wakaondoka, wakarudi kwa Balaki, wakamwambia, “Balaamu amekataa kuja pamoja nasi.”
15. Kisha, Balaki akatuma maofisa wengine, wengi zaidi na wa vyeo vya juu kuliko wale wa kwanza.
16. Hao walifika kwa Balaamu, wakamwambia, “Balaki mwana wa Sipori asema hivi: ‘Usikubali kuzuiwa na chochote hata uache kuja kwangu.
17. Nitakutunukia heshima kubwa, na chochote utakachoniomba nitakutimizia. Njoo uwalaani watu hawa.’”
18. Lakini Balaamu akawajibu watumishi wa Balaki, “Hata kama Balaki atanipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, mimi sitaweza kuvunja amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuhusu jambo lolote, dogo au kubwa.
19. Lakini tafadhalini laleni hapa usiku huu kama wale wenzenu, nami nipate kujua atakachoniambia Mwenyezi-Mungu tena.”
20. Basi, Mungu akamjia Balaamu usiku huo, akamwambia, “Kama watu hawa wamekuja kukuita, nenda pamoja nao, lakini fanya tu kile nitakachokuambia.”
21. Balaamu akaamka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na hao maofisa.
22. Hasira ya Mungu iliwaka kwa sababu Balaamu alikuwa anakwenda; hivyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akakabiliana naye njiani. Wakati huo Balaamu alikuwa amepanda punda wake akiwa na watumishi wake.