5. Mlipotoka Misri niliwaahidi kwamba daima nitakuwa pamoja nanyi. Basi, ningali pamoja nanyi, kwa hiyo, msiogope kitu.
6. “Naam, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema, hivi karibuni nitazitikisa mbingu na dunia, bahari na nchi kavu.
7. Nitayatikisa mataifa yote na hazina zao zote zitaletwa humu, nami nitalifanya hekalu hili kuwa la fahari. Mimi nimesema.
8. Fedha na dhahabu yote duniani ni mali yangu.
9. Hekalu jipya litakuwa lenye fahari zaidi kuliko lile la awali, na mahali hapo ndipo nitakapowapa watu wangu fanaka.” Asema Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
10. Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa tisa, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilimjia nabii Hagai,
11. akamwambia: “Waambie makuhani watoe uamuzi juu ya jambo hili:
12. Kama mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa vazi lake, kisha akagusa kwa upindo wa vazi hilo mkate au chakula kilichopikwa, au divai, au mafuta au chakula cha aina yoyote ile, je, chakula hicho kitakuwa kitakatifu?” Makuhani wakamjibu, “La, hasha.”