9. Lakini kwa sababu ya upendo, ni afadhali zaidi nikuombe. Nafanya hivi ingawa mimi ni Paulo, balozi wa Kristo Yesu, na sasa pia mfungwa kwa ajili yake.
10. Basi, ninalo ombi moja kwako kuhusu mwanangu Onesimo, ambaye ni mwanangu katika Kristo kwani nimekuwa baba yake nikiwa kifungoni.
11. Ni Onesimo yuleyule ambaye wakati mmoja alikuwa hakufai kitu, lakini sasa ananifaa mimi na wewe pia.
12. Sasa namrudisha kwako, naye ni kama moyo wangu mimi mwenyewe.
13. Ningependa akae nami hapa anisaidie badala yako wakati niwapo kifungoni kwa sababu ya Injili.
14. Lakini sitafanya chochote bila kibali chako. Sipendi kukulazimisha unisaidie, kwani wema wako unapaswa kutokana na hiari yako wewe mwenyewe na si kwa kulazimika.
15. Labda Onesimo aliondoka kwako kwa kitambo tu, kusudi uweze tena kuwa naye daima.
16. Na sasa yeye si mtumwa wa kawaida, ila ni bora zaidi ya mtumwa: Yeye ni ndugu yetu mpenzi. Ni wa maana sana kwangu mimi, na kwako atakuwa wa maana zaidi, kama mtumwa na kama ndugu katika Bwana.
17. Basi, ikiwa wanitambua mimi kuwa mwenzako, mpokee tena kama vile ungenipokea mimi mwenyewe.
18. Kama alikuwa amekukosea kitu, au alikuwa na deni lako, basi, unidai mimi.