13. “Ninaamuru kwamba katika utawala wangu, Mwisraeli yeyote, au kuhani wao, au Mlawi, akitaka kurudi Yerusalemu kwa hiari yake, anaweza kwenda pamoja nawe.
14. “Mimi pamoja na washauri wangu saba, tunakutuma uende ufanye uchunguzi huko Yuda na Yerusalemu kuona kama sheria ya Mungu wako ambayo umekabidhiwa inafuatwa kikamilifu.
15. Utachukua fedha na dhahabu ambayo mimi na washauri wangu tumemtolea kwa hiari Mungu wa Israeli ambaye hekalu lake limo mjini Yerusalemu.
16. Utachukua pia fedha na dhahabu yote utakayokusanya katika mkoa wote wa Babuloni, pamoja na matoleo ya hiari waliyotoa Waisraeli na makuhani wao kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.
17. Fedha hiyo utaitumia kwa uangalifu sana kununua mafahali, kondoo dume, wanakondoo na tambiko ya nafaka na divai, na kuvitoa madhabahuni katika nyumba ya Mungu wenu iliyoko Yerusalemu.
18. Fedha na dhahabu itakayobaki unaweza kuitumia pamoja na wananchi wenzako kama mtakavyopenda, kufuatana na mapenzi ya Mungu.