Ezra 4:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha maadui wa watu wa Yuda na Benyamini waliposikia kwamba watu waliorudi kutoka uhamishoni wanalijenga upya hekalu la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli,

2. walimwendea Zerubabeli na viongozi wa koo, na kumwambia, “Tafadhali tushirikiane katika ujenzi wa hekalu. Sisi kama nyinyi tunamwabudu Mungu wenu, na tumekuwa tukimtolea tambiko tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru aliyetuleta hapa.”

3. Lakini Zerubabeli, Yeshua na viongozi wengine wa koo za Israeli wakawaambia, “Sisi hatuhitaji msaada wowote kutoka kwenu ili kuijenga nyumba ya Mungu wetu. Sisi wenyewe tutamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kama mfalme Koreshi wa Persia alivyotuamuru.”

4. Hapo, watu waliokuwa wanaishi mahali hapo wakaanza kuwavunja moyo na kuwatisha Wayahudi ili wasiendelee kama walivyokusudia.

5. Tena waliwahonga maofisa wa serikali ya Persia wawapinge Wayahudi. Waliendelea kufanya hivyo muda wote wa utawala wa Koreshi, mpaka wakati wa utawala wa Dario.

6. Mwanzoni mwa utawala wa mfalme Ahasuero, maadui wa watu waliokaa Yuda na Yerusalemu waliandika mashtaka dhidi yao.

7. Tena wakati wa utawala wa Artashasta, mfalme wa Persia, Bishlamu, Mithredathi, Tabeeli na rafiki zao, walimwandikia barua mfalme Artashasta. Barua hiyo iliandikwa kwa herufi za Kiaramu na kutafsiriwa.

8. Pia mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa, walimwandikia Artashasta barua ifuatayo dhidi ya Yerusalemu:

9. “Kutoka kwa mtawala Rehumu na Shimshai, katibu wa mkoa pamoja na wenzetu, na mahakimu, maofisa wote ambao hapo awali walitoka Ereki, Babuloni na Susa katika nchi ya Elamu,

10. pamoja na watu wa mataifa mengine ambao Asur-banipali, mtu mkuu na mwenye nguvu aliwahamisha na kuwaweka katika mji wa Samaria na mahali pengine katika mkoa wa magharibi ya Eufrate.”

Ezra 4