8. Nilitazama, nikaona ile mifupa imewekewa mishipa na nyama na kufunikwa kwa ngozi. Lakini haikuwa na uhai.
9. Hapo, Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Ewe mtu, kwa niaba yangu toa unabii kwa upepo, ukauambie kwamba Bwana Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Ewe upepo njoo toka pande zote nne na kuipuliza miili hii iliyokufa ili ipate kuishi.”
10. Basi, mimi nikatoa unabii kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikaingia ndani yao, nayo ikawa hai, ikasimama: Kundi kubwa ajabu.
11. Hapo Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu! Mifupa hiyo ni watu wote wa Israeli. Wao, wanasema, ‘Mifupa yetu imenyauka, matumaini yetu yamepotea nasi tumekwisha kabisa.’
12. Kwa hiyo, toa unabii, uwaambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwafufua kutoka makaburini mwenu. Nitawarudisha nyumbani kwenu katika nchi ya Israeli.