5. Mji wa Raba nitaufanya kuwa malisho ya ngamia na nchi ya Amoni zizi la kondoo. Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
6. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa sababu mlipiga makofi, mkarukaruka kwa furaha na kushangilia sana juu ya nchi ya Israeli,
7. basi, mimi nimeunyosha mkono dhidi yenu; nitawaacha mtekwe nyara na watu wa mataifa mengine. Nitawaangamizeni, nanyi hamtakuwa taifa tena wala kuwa na nchi. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”
8. Bwana Mwenyezi-Mungu alisema: “Kwa kuwa Moabu imesema kuwa Yuda ni sawa tu na mataifa mengine,
9. mimi nitaifanya miji inayolinda mipaka ya Moabu ishambuliwe, hata miji ile bora kabisa, yaani Beth-yeshimothi, Baal-meoni na Kiriathaimu.
10. Nitaitia nchi hiyo pamoja na nchi ya Amoni mikononi mwa watu wa mashariki iwe mali yao. Nchi ya Moabu haitakuwa taifa tena.