Ezekieli 24:10-26 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Nitaleta magogo ya kuni na kuwasha moto. Nitachemsha nyama vizuri sana. Nitachemsha na kukausha mchuzi, na mifupa nitaiunguza!

11. Hicho chungu kitupu nitakiweka juu ya makaa kipate moto sana, shaba yake ipate moto, uchafu wake uyeyushwe na kutu iunguzwe.

12. Lakini najisumbua bure; kutu yake nene haitoki hata kwa moto.

13. Ewe Yerusalemu, matendo yako machafu yamekutia unajisi. Ingawa nilijaribu kuutakasa, wenyewe ulibaki najisi. Basi, hutatakasika tena mpaka nitakapoitosheleza hasira yangu juu yako.

14. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Jambo hilo litakamilika; mimi nitalitenda. Sitaghairi jambo hilo wala kukuonea huruma. Nitakuadhibu kulingana na mwenendo na matendo yako. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

15. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

16. “Wewe mtu! Tazama, kwa pigo moja nitakuondolea mpenzi wako. Lakini usiomboleze, wala kulia, wala kutoa machozi.

17. Utasononeka, lakini sio kwa sauti. Hutamfanyia matanga huyo aliyekufa. Vaa viatu vyako na kuvaa kilemba; usiufunike uso wako wala kula chakula cha matanga.”

18. Basi, asubuhi nilizungumza na watu, na jioni mke wangu akafariki. Na kesho yake asubuhi, nilifanya kama nilivyoamriwa.

19. Watu wakaniuliza: “Je, jambo hili unalofanya lamaanisha nini kwetu?”

20. Nikawajibu, “Mwenyezi-Mungu aliniagiza

21. niwaambie nyinyi Waisraeli kwamba Mwenyezi-Mungu ataitia unajisi maskani yake, hiyo nyumba ambayo ni fahari ya ukuu wenu, na ambayo mnafurahi sana kuiona. Nao watoto wenu, wa kiume kwa wa kike, mliowaacha nyuma watauawa kwa upanga.

22. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya. Hamtazifunika nyuso zenu wala kula chakula cha matanga.

23. Mtavaa vilemba vyenu na viatu miguuni; hamtaomboleza, wala kulia. Kutokana na maovu yenu, mtadhoofika na kusononeka, kila mtu na mwenzake.

24. Nami Ezekieli nitakuwa ishara kwenu: Mtafanya kila kitu kama nilivyotenda. Wakati mambo hayo yatakapotukia, mtatambua kuwa yeye ndiye Bwana Mwenyezi-Mungu.”

25. Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Wewe mtu! Siku ile nitakapoondoa kwao hicho ambacho ni tegemeo lao, na sababu ya shangwe yao, mahali ambapo wanapenda sana kupaona, nitawaondoa watoto wao wa kiume na wa kike.

26. Siku hiyo, mtu atakayeokoka atakuja kukupasha habari hizo.

Ezekieli 24