Ezekieli 11:5-11 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Kisha roho ya Mwenyezi-Mungu ikanijia, naye akaniambia, “Waambie watu, Mwenyezi-Mungu asema hivi: Naam, hiki ndicho mnachofikiri enyi Waisraeli. Najua mambo mnayofikiria moyoni mwenu.

6. Nyinyi mmewaua watu wengi mjini humu, na kujaza barabara zake na watu waliouawa.

7. “Lakini, mimi, Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Naam, mji huu ni chungu cha kupikia, na wale waliouawa ndio nyama. Nyinyi lazima mtaondolewa mjini.

8. Nyinyi mmeogopa upanga? Basi, mimi nitaleta upanga dhidi yenu!

9. Nitawatoa ndani ya mji na kuwatia mikononi mwa watu wa mataifa mengine, nami nitawahukumu.

10. Mtauawa kwa upanga, nami nitawahukumu mpakani mwa Israeli. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

11. Mji wa Yerusalemu hautakuwa tena chungu chenu wala nyinyi hamtakuwa nyama ndani yake. Mimi nitawahukumu mpakani mwa Israeli.

Ezekieli 11