Ezekieli 1:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Katikati ya hao viumbe hai kulikuwa na kitu kilichoonekana kama makaa yanayowaka moto, kama miali ya moto iliyomulika huku na huko kati ya hao viumbe. Moto huo ulikuwa mwangavu na umeme ulichomoza humo.

14. Viumbe hao pia walikwenda huku na huko kama pigo la umeme.

15. Nilipokuwa nawatazama hao viumbe hai niliona chini karibu na kila kiumbe kulikuwa na gurudumu.

16. Magurudumu hayo yalionekana kuwa ya namna moja, yanametameta kama jiwe la zabarajadi na muundo wao ulikuwa kama gurudumu ndani ya gurudumu lingine.

17. Yaliposogea yalikwenda upande wowote wa pande nne za dira ya dunia bila kugeuka.

18. Mizingo ya hayo magurudumu ilikuwa mirefu kutisha na mizingo ya magurudumu hayo ilikuwa imejaa macho pande zote.

19. Hao viumbe hai walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda kandokando yao; na viumbe hao walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu hayo yaliinuka.

20. Popote roho ilipokwenda walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja nao; maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo.

21. Viumbe hao walipokwenda, magurudumu nayo yalikwenda; waliposimama, nayo yalisimama; walipoinuka juu kutoka ardhini, magurudumu nayo yaliinuka pamoja nao. Maana roho ya hao viumbe hai ilikuwa katika magurudumu hayo.

22. Juu ya vichwa vya hao viumbe hai kulikuwa na kitu mfano wa anga, kinangaa kama kioo.

23. Chini ya kitu hicho walisimama hao viumbe hai; mabawa mawili ya hao viumbe yalikuwa yamekunjuliwa kuelekeana, na kwa mabawa mengine mawili walifunika miili yao.

24. Walipokuwa wanakwenda, nilisikia sauti ya mabawa yao; sauti ya mvumo huo ilikuwa kama ile ya maji mengi, kama sauti ya ngurumo kutoka kwa Mungu wa majeshi, na kama kelele ya jeshi kubwa. Waliposimama, walikunja mabawa yao.

Ezekieli 1