12. Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero.
13. Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu.
14. Jioni ulikuwa ndio wakati wa kwenda, na kesho yake asubuhi, mwali huyo alipelekwa katika nyumba nyingine ya wanawake, chini ya Shaashgazi, towashi msimamizi wa masuria wa mfalme. Mwali haikumpasa kurudi kwa mfalme, isipokuwa kama mfalme amependezwa naye kiasi cha kuagiza aitwe kwa jina.
15. Wakati uliwadia wa Esta kwenda kwa mfalme. Huyo, binti Abihaili, binamu ya Mordekai, na ambaye alilelewa na Mordekai, hakuomba chochote zaidi ya kile alichopangiwa na Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wa mfalme. Kila mtu aliyemwona Esta, alipendezwa naye.