10. Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo.
11. Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.
12. Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero.
13. Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu.