1. Baadaye, hasira yake ilipokwisha tulia, mfalme Ahasuero alimkumbuka Vashti, akawa anatafakari juu ya ukaidi wake na hatua iliyochukuliwa dhidi yake.
2. Basi, watumishi wake, waliokuwa wanamhudumia yeye binafsi, wakamshauri, “Kuna wasichana wengi wazuri; kwa nini usitafutiwe mmoja?
3. Unaweza kuteua maofisa katika kila mkoa wa utawala wako, na kuwaagiza wawalete wasichana wazuri wote kwenye nyumba ya wanawake hapa Susa, mji mkuu. Halafu wawekwe chini ya uangalizi wa Hegai, towashi mwangalizi wa wanawake wako; na hapo wapewe mafuta na vifaa vingine ili wajirembeshe zaidi.
4. Yule atakayekupendeza zaidi, na afanywe malkia badala ya Vashti.” Mfalme akaona shauri hilo ni jema, akafanya hivyo.
5. Mjini Susa, palikuwa na mtu mmoja Myahudi, jina lake Mordekai, mwana wa Yairi mwana wa Shimei, mwana wa Kishi wa kabila la Benyamini.
6. Mordekai alikuwa miongoni mwa watu wale waliochukuliwa mateka wakati mfalme Yekonia wa Yuda alipotekwa na mfalme Nebukadneza wa Babuloni.