18. Basi, mjumbe huyo alipokwenda alikutana na Yehu na kumwambia, “Mfalme anauliza: Kuna amani?” Yehu akajibu, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!” Mlinzi juu ya mnara akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini harudi.”
19. Ndipo mjumbe wa pili akatumwa, ambaye pia alimwuliza Yehu swali hilohilo. Yehu akamwambia vivyo hivyo, “Kwa nini unauliza kuhusu amani? Wewe geuka ufuatane nami!”
20. Kwa mara nyingine tena mlinzi akasema “Mjumbe amewafikia lakini harudi.” Halafu akaongeza, “Uendeshaji wa gari ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi; kwa sababu yeye huendesha kwa kasi.”
21. Basi, Yoramu mfalme wa Israeli akaamuru akisema, “Tayarisha gari.” Nao walitayarisha gari lake. Kisha Yoramu mfalme wa Israeli na Ahazia mfalme wa Yuda waliondoka kila mmoja akipanda gari lake, wakaenda kukutana na Yehu. Walimkuta katika uwanja wa Nabothi Myezreeli.
22. Ikawa Yoramu, alipomwona Yehu, alimwuliza, “Je, kuna amani, Yehu?” Yehu akamjibu, “Amani gani, wakati makahaba na wachawi wa Yezebeli ni wengi?”