1. Basi, wewe mwanangu, uwe na nguvu katika neema tunayopata katika kuungana na Kristo Yesu.
2. Chukua yale mafundisho uliyonisikia nikitangaza mbele ya mashahidi wengi, uyakabidhi kwa watu wanaoaminika, ambao wataweza kuwafundisha wengine pia.
3. Shiriki katika mateso kama askari mwaminifu wa Kristo Yesu.
4. Mwanajeshi vitani hujiepusha na shughuli za maisha ya kawaida, ili aweze kumpendeza mkuu wa jeshi.
5. Mwanariadha yeyote hawezi kushinda na kupata zawadi ya ushindi kama asipozitii sheria za michezo.
6. Mkulima ambaye amefanya kazi ngumu anastahili kupata sehemu ya kwanza ya mavuno.
7. Fikiria hayo ninayosema, kwani Bwana atakuwezesha uelewe kila kitu.
8. Mkumbuke Yesu Kristo aliyefufuliwa kutoka kwa wafu, aliyekuwa wa ukoo wa Daudi, kama isemavyo Habari Njema ninayoihubiri,
9. na ambayo kwa sababu yake mimi nateseka na nimefungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu haliwezi kufungwa minyororo.
10. Kwa hiyo navumilia kila kitu kwa ajili ya wateule wa Mungu, ili wao pia wapate ukombozi upatikanao kwa njia ya Yesu Kristo, na ambao huleta utukufu wa milele.