18. Wana watatu wa Seruya: Yoabu, Abishai na Asaheli walikuwapo hapo. Asaheli alikuwa na mbio kama paa.
19. Asaheli alimfuatia Abneri moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto.
20. Abneri alipoangalia nyuma na kumwona Asaheli, alimwambia, “Je, ni wewe Asaheli?” Yeye akamjibu, “Naam, ni mimi.”
21. Abneri akamwambia, “Geukia kulia au kushoto, umkamate kijana mmoja na kuchukua nyara zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfuatia.
22. Abneri akamwambia Asaheli mara ya pili, “Acha kunifuatia. Kwa nini nikuue? Nitawezaje kuonana na kaka yako Yoabu?”