4. Akasema, “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwani kwa nguvu yake ameitimiza ahadi yake aliyoitoa kwa baba yangu Daudi akisema,
5. ‘Tangu niwaondoe watu wangu kutoka nchi ya Misri, sikuchagua mji wowote katika makabila ya Israeli ili nijengewe nyumba nitakamoabudiwa; na sikumchagua mtu yeyote awe mkuu wa watu wangu Israeli.
6. Nimeuchagua mji wa Yerusalemu uwe mji ambamo nitaabudiwa, na nimemchagua Daudi awatawale watu wangu Israeli.’
7. “Kwa hiyo, baba yangu Daudi alikusudia kujenga nyumba atakamoabudiwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.
8. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia baba yangu Daudi, ‘Ni vyema kwamba ulikusudia moyoni mwako kunijengea nyumba.
9. Hata hivyo, si wewe utakayejenga hiyo nyumba, ila mwanao utakayemzaa ndiye atakayenijengea hiyo nyumba.’”