1. Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; alitawala miaka thelathini na mmoja huko Yerusalemu.
2. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu. Alifuata njia zake Daudi babu yake, na kushika amri za Mwenyezi-Mungu kwa dhati.
3. Katika mwaka wa nne wa utawala wake, mfalme Yosia, akiwa bado kijana, alianza kumwabudu Mungu wa Daudi, baba yake. Baadaye alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili alianza kuisafisha Yuda na Yerusalemu kwa kuharibu mahali pa kuabudia miungu mingine, sanamu za Ashera, na sanamu nyinginezo za kuchonga na za kusubu.